1 Kings 10:1-13

Malkia Wa Sheba Amtembelea Solomoni

(2 Nyakati 9:1-12)

1 aMalkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la Bwana, akaja kumjaribu kwa maswali magumu. 2 bAlifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. 3 cSolomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea. 4 dMalkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, 5 echakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika hekalu la Bwana, alipatwa na mshangao.

6 fAkamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. 7Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. 8 gHeri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako! 9 hAhimidiwe Bwana Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake Bwana wa milele ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”

10Naye akampa mfalme talanta 120
Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5.
za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni.

11 j(Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani. 12 kMfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo ya Hekalu la Bwana na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa au kuonekana humo tangu siku ile.)

13Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

Copyright information for SwhNEN